Friday, June 7, 2013

Ccm yatabiliwa mabaya mbele ya Wassira


Kampeni-Wasira-1
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Dk Charles Kitima amekitabiria kifo Chama Cha Mapinduzi kama kitaendelea na mtindo wa kuwanyima fursa wazawa katika maendeleo.

Akizungumza katika kongamano la kujadili amani na maendeleo na mpango wa miaka mitano wa kukuza uchumi na kuondoa umaskini nchini lililofanyika chuoni hapo jijini Mwanza, Dk Kitima alisema nchi haiwezi kufikia dira ya maendeleo ikiwa Serikali imeshindwa kutoa kipaumbele katika utawala mzuri wa rasilimali na wazawa:
“CCM isipojirekebisha itakufa mapema kama isipoipa kipaumbele sekta binafsi ya wazawa katika kusimamia rasilimali ya nchi.Tunataka rasilimali za nchi tusimamie wenyewe,” alisema Charles Kitima.
Akizungumza mbele ya Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Uhusiano na Urtatibu, Steven Wassira aliyekuwa mgeni rasmi, aliongeza kuwa nchi itaendelea kwa kuwapa fursa wananchi wake.
Kwa upande wake Waziri Wassira alikiri kuwa umaskini wa Tanzania unasababishwa na kutokuwapo kwa uzalendo, kupungua kwa uadilifu na mfumo mbovu ya ufuatiliaji na utekelezaji wa mipango. “Uadilifu umekuwa mdogo sana kwa viongozi wetu wa leo. Mawazo yaliyotawala ni wizi tu na mimi sina mpango wa kuiba”alisema Wassira.
Hata hivyo Wassira alisema kutokuwa na uelewa tulikotoka nayo ni sababu kubwa kwa wananchi kutokujua maendeleo yaliyofikiwa kwa miaka 50 ya uhuru.
“Tanzania ni nchi tuliyoirithi ikiwa ni shamba tu hatukukuta kitu. Hapakuwa na barabara za kutosha, elimu haikupewa kipaumbele, kutoka wasomi wachache wa mwaka 1961 sasa kuna vyuo 44’’ alisema.
Naye Mhadhiri wa Sheria chuoni hapo, Adelardius Kilange alisema tatizo la umaskini nchini linatokana na wananchi kukosa misingi imara ya itikadi ya siasa na uchumi wa jamii na kwamba ipo haja kwa Serikali kujipanga.

0 comments:

Post a Comment