Kutokana na rasimu ya Katiba Mpya kupendekeza kufutwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu, rasimu hiyo inapendekeza waziri yeyote mwandamizi ateuliwe kukaimu nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa rais na makamu wake hawapo nchini kutokana na sababu zozote zile. Mapendekezo hayo ni tofauti na Katiba ya sasa ambayo inatamka kwamba ikiwa Rais na Makamu wake hawapo, basi nafasi hiyo ya juu katika nchi itashikwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Mkuu aliwekwa katika orodha ya wanaoweza kukaimu nafasi hiyo
katika marekebisho ya Katiba yaliyofanywa mwaka 2000 kupitia waraka
maalumu wa Serikali (white paper) na baadaye kupitishwa na Bunge.
Kabla ya marekebisho hayo ya 13, Ibara ya 37(3)(a) na (b) ilikuwa
ikieleza kuwa iwapo Rais na Makamu wake hawapo nafasi hiyo ilitakiwa
kushikiliwa na Spika wa Bunge na kama hayupo basi Jaji Mkuu wa Tanzania
ndiye alitakiwa kukaimu nafasi hiyo.
Lakini mapendekezo ya Rasimu ya Katiba Mpya katika Ibara ya
73(1)(b)na (c) inaeleza kuwa endapo Rais na Makamu wake hawatakuwapo
basi nafasi hiyo itashikiliwa na waziri mwandamizi na kama hatakuwapo
basi Baraza la Mawaziri ndilo litakalokuwa na dhamana ya kuchagua mtu wa
kukaimu nafasi hiyo.
Hata hivyo, mtu yeyote atakayekaimu nafasi ya madaraka ya Rais, kwa
namna yoyote ile, hatakuwa na madaraka ya kuteua au kumwondoa madarakani
kiongozi yeyote yule aliyeteuliwa na Rais kwa mujibu wa Katiba au jambo
jingine lolote kama litakavyoainishwa na Rais katika hati ya kukasimu
madaraka yake.
“Rais atakasimu madaraka yake kwa hati maalumu aliyotia saini yake,”
inaelekeza rasimu hiyo iliyozinduliwa Jumatatu wiki hii na Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Kadhalika rasimu hiyo inaeleza kuwa endapo Baraza la Mawaziri litaona
kuwa Rais hawezi kumudu kazi zake kwa sababu ya maradhi ya mwili au
akili, linaweza kuandaa azimio la kumwomba Jaji Mkuu athibitishe kwamba
Rais, kwa sababu ya maradhi ya mwili au ya akili, hawezi kumudu kazi
zake.
“Baada ya kupokea azimio hilo, atateua bodi ya utabibu ambayo
itachunguza suala hilo na kumshauri Jaji Mkuu ipasavyo,” inaelekeza
rasimu hiyo.
Jaji Mkuu baada ya kutafakari ushauri na ushahidi wa kitabibu,
atampelekea Spika hati ya kuthibitisha kwamba kutokana na maradhi ya
mwili au akili, Rais ameshindwa kumudu kazi zake, na iwapo Jaji Mkuu
hatabatilisha hati hiyo ndani ya siku saba kutokana na Rais kupata nafuu
na kurejea kazini, basi itahesabiwa kwamba kiti cha Rais kipo wazi.
Kutokana na hali hiyo, bodi ya utabibu itakayoteuliwa kwa mujibu wa
Katiba itajumuisha watu wasiopungua watatu kutoka miongoni mwa madaktari
bingwa wanaotambuliwa na sheria inayohusu madaktari ya Tanzania.
“Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia,
kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi, kutomudu kazi zake kutokana na
maradhi ya mwili au akili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za
Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na kushika madaraka ya Rais kwa
muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano,” inaeleza sehemu nyingine
ya rasimu hiyo.
Pia rasimu hiyo imeelezea kuwapo kwa Mawaziri Wakaazi ambao kila
Mshirika wa Muungano atateua Waziri Mkaazi atakayeratibu na kusimamia
uhusiano baina ya Serikali za Washirika na kati ya Serikali ya Mshirika
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
“Mawaziri Wakaazi watakuwa na ofisi zao na watafanya kazi wakiwa
Makao Makuu ya Serikali ya Muungano na pamoja na majukumu mengine
watakayopangiwa na Serikali za Washirika wa Muungano,” imeeleza ibara ya
64 ya rasimu hiyo.
Inasema Mawaziri Wakaazi watakuwa na majukumu ya kushughulikia mambo
yasiyo ya Muungano yanayohusu ushirikiano au uhusiano wa kimataifa; na
kuwa kiungo baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali za
Washirika wa Muungano na baina ya Serikali za Washirika wa Muungano.
0 comments:
Post a Comment