Tuesday, June 17, 2014

Tazama Watoto walia kwa majonzi!!

Jina la mtoto Nasra Mvungi jana lilitawala maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika nchini. Watoto walielezea kilio chao .

juu ya ukatili unaofanywa na wazazi na walezi wao wakirejea mateso aliyoyapata marehemu Nasra aliyeishi kwenye boksi kwa miaka takriban mitatu huko Morogoro.
Mkoani Dar es Salaam; watoto walisimama kwa dakika moja kumkumbuka Nasra, pamoja na watoto wengine waliopoteza maisha kutokana na ukatili. Walisimama wakati watoto, Given Godfrey na Mariam Yusuph walipokuwa wakisoma risala kwa mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi. Walieleza baadhi ya vitendo vya ukatili ambavyo watoto wanakumbana navyo kutoka kwa wazazi na walezi wao wakitoa mfano wa jinsi Nasra alivyoteseka kwa kufungiwa na kuishi ndani ya boksi.
“Wazazi na walezi wetu wamegeuka maadui kwetu kwani ndiyo wanaoongoza kwa kutufanyia vitendo vya ukatili… naomba tusimame kwa dakika moja tumkumbuke mtoto mwenzetu Nasra aliyefariki kutokana na kutengwa tena na ndugu zake wa karibu na kuishi kwenye boksi kwa miaka mitatu.”
Mbali na vitendo vya ukatili, watoto hao walilalamikia ukosefu mkubwa wa madawati, vitabu vya kiada, vyoo na walimu katika shule nyingi nchini, jambo ambalo walisema linawakwamisha upatikanaji wa elimu bora kama kaulimbiu ya mwaka huu inavyosema: “Kupata elimu bora isiyo na vikwazo ni haki ya kila mtoto.”
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mushi aliwataka wazazi na jamii kwa jumla kuhakikisha inalinda na kutetea haki za watoto tofauti na inavyoonekana sasa kwa wengi wao kugeuka kuwa maadui kwa kuwatesa na kuwanyanyasa.
“Wazazi wamekuwa wakiwafanyia vitendo viovu watoto mithili ya wanyama hali iliyowafanya wawaogope watu wazima kuliko wanavyoogopa wanyama. Hii haina budi kubadilika,” alisema Mushi na kuongeza: “Kila mtoto ana haki ya kupendwa, kulindwa, kuishi na kupata elimu bora hivyo ni lazima kila mzazi ahakikishe anatimiza wajibu wake.”
Kibaha
Katika Wilaya ya Kibaha, watoto kutoka shule mbalimbali wameuomba uongozi wa wilaya hiyo kuweka sheria madhubuti ya kuwabana baadhi ya wazazi wanaowaruhusu watoto wao kwenda kukesha kwenye ngoma za usiku hali inayosababisha madhara ikiwamo kupata mimba.
Katika risala yao iliyosomwa na watoto hao kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Halima Kihemba walisema sasa wapo baadhi ya wazazi wanaowaruhusu watoto wao kushiriki ngoma za usiku jambo linalokwenda kinyume na haki ya kumlinda mtoto.
Pia walisema kuwa bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kielimu ikiwamo kukosa fursa kwa makundi yaliyo pembezoni, vifaa ya kusomea na kujifunzia zenye ubora pamoja na miundombinu isiyoridhisha kwenye madarasa yao.
Wasikitishwa na ukatili
Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) yamesikitishwa na ukatili wanaofanyiwa watoto na kutaka hatua kali za kisheria kuchukuliwa.The superonenews.blogspot.com

0 comments:

Post a Comment