Wednesday, June 12, 2013

SAKATA LA ROONEY NA MAN UNITED, BADO NI KIZUNGUMKUTI!!!

ROONEY_NA_FERGIEJULAI 3 KIKOSI cha Mabingwa Manchester United kitakusanyika tena ndani ya Carrington, Kituo cha Mazoezi yao Jijini Manchester, na pengine Straika Wayne Rooney atakuwepo licha ya uvumi mzito wa yeye kuhama.
Uvumi huu wa kuhama kwa Rooney, mwenye Miaka 27, ulishika hatamu pale Sir Alex Ferguson, ambaye sasa ni Meneja Mstaafu, alipodokeza kuwa Rooney alimfuata na kuonyesha nia yake kutaka kuihama Klabu hiyo hasa baada ya kutopangwa Mechi muhimu ikiwemo ile ya UEFA CHAMPIONS LIGI dhidi ya Real Madrid Mwezi Machi na pia kupigwa Benchi Mechi kadhaa zilizofuatia.
Lakini, mwenyewe Rooney pamoja na kambi yake ya Washauri, imekataa kabisa kuwa Mchezaji huyo hakuwa na nia ya kuihama Manchester United.
Hadi hii leo si Rooney wala Msemaji wake yeyote alietamka kinagaubaga kuwa Staa huyo anataka kuipa teke Old Trafford.
Mwezi Oktoba 2010, Wayne Rooney aliwahi kuitaka Man United imruhusu kuhama lakini, baada ya majadiliano na makubaliano ya haraka haraka, akaongezewa Mshahara na kufikia Pauni 250,000 kwa Wiki na kupewa Mkataba mpya wa Miaka mitano.
Wakati huo, wakati hali ikiwa tete, Kundi la Mashabiki wa Man United walizingira Nyumba yake na kumpa vitisho na Siku ya pili yake tu Man United ikatamka Rooney anasaini Mkataba mpya.
Mara baada ya Sir Alex Ferguson kudokeza kuwa Rooney anataka kuhama, Man United, kama Klabu, ilitoa tamko rasmi kuwa Mchezaji huyo, ambae Mkataba wake unamalizika Mwaka 2015, hauzwi.
Tamko hilo lilifuatia kuibuka kwa shamrashamra za Klabu mbalimbali kutaka kumsaini ikiwemo hata Arsenal ambayo haisifiki kwa kununua Wachezaji wa ‘Bei kubwa’
Sasa Sir Alex Ferguson hayuko tena kwenye picha na Meneja mpya ni David Moyes ambae ndio Mtu alieibua kipaji cha Wayne Rooney wakati wakiwa nae Everton kwa kumpa nafasi kucheza Timu ya Kwanza akiwa na Miaka 16 tu.

0 comments:

Post a Comment