Utata umeibuka
kuhusu wabunge waliotajwa kwenye ripoti ya Kamati ndogo ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira kuwa wanahusika na biashara ya pembe za
ndovu.
Wakati Ofisi ya Bunge ikidai kuwa ripoti hiyo
haina majina ya wabunge, Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli
ameshikilia kuwa majina hayo ni sehemu ya ripoti hiyo ambayo baada ya
kuwasilishwa, iliibua mjadala ambao ulisababisha mawaziri wanne
kuong’oka.
Gazeti hili limedokezwa kuwa majina ya wabunge hao
yalitajwa mbele ya kamati hiyo wakati ikichunguza jinsi Operesheni
Tokomeza Ujangili ilivyotekelezwa, baada ya kuwapo kwa malalamiko ya
vitendo vya ukatili na utesaji wa raia.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa hizo, wabunge
hao hawakuitwa mbele ya kamati hiyo kuhojiwa kutokana na kwamba suala
hilo halikuwa moja ya hadidu za rejea walizopewa kuzitafutia majawabu.
“Sisi tulimaliza kazi na kuikabidhi Ofisi ya
Bunge, ni kweli majina hayo hayamo kwenye ripoti (iliyosomwa bungeni)
lakini nilikuwa navyo kwenye viambatanisho na ushahidi wake,” alisema
Lembeli jana.
Alipoulizwa sababu za kutokuweka majina ya wabunge
hao katika taarifa iliyosomwa bungeni Desemba 20, mwaka jana, mbunge
huyo wa Kahama alisema: “Hiyo haikuwa kazi yetu sisi tulikuwa na wajibu
wa kueleza yaliyotokana na Operesheni Tokomeza tu, lakini hayo mengine
yapo kwenye viambatanisho.”
Ripoti ya kamati ndogo iliweka bayana jinsi watu
mbalimbali walivyoteswa na vyombo vya dola wakati wa operesheni hiyo na
baada ya mjadala bungeni, Rais Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wa
mawaziri hao.
Mawaziri wanne walioachishwa ni pamoja na Dk
Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT),
Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Dk Mathayo David
(Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi).
Ofisa wa Bunge, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina
lake alisema taarifa iliyowasilishwa bungeni siku hiyo haikutaja majina
ya wabunge hao na kwamba hata kwenye Hansard (taarifa za Bunge), za siku
ya mjadala huo suala hilo halimo.
“Wabunge ni kama walifanya makosa, baada ya
mwenyekiti (Lembeli) kusema kwamba wabunge wanatajwa kwa ujangili,
walipaswa kutumia kanuni maana zipo, kutaka majina yao yatajwe,” alisema
ofisa huyo.
Kauli yake iliungwa mkono na Naibu Spika, Job
Ndugai ambaye alisema: “Kimsingi kwa mujibu wa taratibu za Bunge,
taarifa inayowasilishwa bungeni ndiyo inayosomwa na ni wazi kwa umma,
haiwi siri.”
Ndugai alisema katika mazingira hayo, isingekuwa siri kama majina hayo yangetajwa kwenye taarifa ya kamati. posted by http://thesuperonenews.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment