Wednesday, August 7, 2013

TEVEZ AKATA TAMAA NA ARGENTINA, NUSURA ASTAAFU SOKA!!

CARLOS_TEVEZ-AUG7
STAA kutoka Argentina Carlos Tevez amekataa tamaa kabisa ya kurudi kwenye Timu ya Taifa ya Argentina na nusura astaafu Soka kama si kutokea Juventus ya Italy iliyomnunua Mwezi Juni.
Akiongea kwenye Mahojiano na Kituo cha TV cha ESPN cha Mtandao wa Nchi za Marekani ya Kusini, Tevez alisema kuwa upo uhakika kuwa muda wake wa kuichezea Argentina sasa umekwisha.
Kwa sasa Argentina wapo njiani kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2014 huko Nchini Brazil wakiwa wapo kwenye kilele cha Kundi la Kanda ya Nchi za Marekani ya Kusini.
Tevez amezungumza: “Imekwisha. Nimesema nilichosema kuhusu Timu ya Taifa na sina la ziada!”
Tevez, Miaka 29, hajaichezea Argentina tangu Alejandro Sabello ateuliwe kuwa Kocha wa Nchi hiyo Miaka miwili iliyopita.
Tevez amenena: “Nilisema ukweli, nilisema nilichokuwa na hisia nacho na huo ni mwisho. Nikiongelea kuhusu hili itaonekana kama naomba nirudishwe tena.”
Tevez alikaa Miaka minne na Manchester City na kukumbwa na migogoro kadhaa ikiwa pamoja na kugombana hadharani na Meneja Roberto Mancini Septemba 2011 alipokataa kupasha moto ili aingizwe kucheza Mechi ya UEFA CHAMPIONZ LIGI na Bayern Munich.
Tevez, ambae pia alizichezea West Ham na Man United, ameongea: “Siku zote nilisema nitastaafu nikiwa na Miaka 28 na ilikuwa karibu kabisa kufanya hivyo nilipogombana na Roberto. Pia nilikuwa nimechoka. Nilikaa Miaka 6 England na hakuna alietegemea hilo. Nilishinda UEFA CHAMPIONZ LIGI nikiwa na United, Ligi Kuu nikiwa United, FA Cup na City, nilishinda kila kitu!”
Aliongeza: “Kuna wakati unachoka, unachoka Soka. Nilitaka kuacha Soka na mara Juventus wakaja, hii ni moja ya Timu kubwa Ulaya!”

0 comments:

Post a Comment