Uongozi wa klabu ya Real Madrid umethibitisha kuidhinishwa kwa paundi milioni 85 za kumnunua Gareth Bale toka Tottenham Hotspurs. Ofa hiyo itaifunika ofa ya paundi milioni 80 ambazo Madrid ilitumia kumnunua Cristiano Ronaldo toka Manchester United .
Mkurugenzi mpya wa Real Madrid ambaye masuala yote ya usajili yako chini yake , Zinedine Zidane alinukuliwa akisema kuwa Real iko tayari kuvunja rekodi ya usajili kwa ajili ya winga huyo ambaye alimaliza msimu uliopita kama mchezaji bora wa ligi kuu ya England baada ya kukusanya tuzo tatu kwenye ligi hiyo .
Bale aling’aa akiwa na klabu yake ya Spurs ambapo alifunga mabao 19 kwenye ligi kuu ya England huku akichangia mabao yaliyofungwa na wachezaji wenzie, kiwango chake ambacho kimekuwa kikipanda siku hadi siku hasa baada ya kubadilishwa nafasi toka kuwa winga hadi kucheza kama mshambuliaji kitu ambacho kimeongeza thamani yake .
Taarifa nyingine zinadai kuwa kushindwa kwa klabu ya Spurs kufuzu kushiriki michuano ya UEFA Champions League kumemfanya Gareth Bale atamani kuondoka kwenye klabu hiyo na Real Madrid wamekuwa wakiongoza orodha ya timu zinazomhitaji.
Rais wa Real , Florentino Perez alisema kuwa mchezaji huyo amezaliwa kuichezea Real na atahakikisha kuwa anatua Madrid kuiongeza nguvu safu yake ya ushambuliaji.
Endapo Real itamnunua Bale itakuwa inavunja rekodi ya bei ya mchezaji kwa mara yake ya tano baada ya kufanya hivyo kwa wachezaji Luis Figo , Zinedine Zidane , Ricardo Kaka na Cristiano Ronaldo.
0 comments:
Post a Comment