KLABU
ya soka ya Simba haikuweza kufanya vizuri msimu uliopita katika Ligi Kuu ya
Tanzania Bara, kwani kutoka bingwa mtetezi iliambulia nafasi ya tatu msimu
uliopita na kuiacha Yanga ikitwaa ubingwa.
Hadi
kutwaa nafasi ya tatu, Simba ilipambana vilivyo kwani Kagera Sugar nayo ilikuwa
ikiwania nafasi hiyo kwa udi na uvumba. Jitihada za wachezaji na benchi la
ufundi ndizo zilizoifanya Simba kutwaa nafasi ya tatu.
Usajili
ukiwa unaendelea, Simba imeshamsajili kipa Andrew Ntala kutoka Kagera Sugar,
huku tayari ikiwa na makipa Juma Kaseja na Abel Dhaira. Usisahau yule wa kikosi
cha pili cha timu hiyo.
Wakati
Simba ikilundika makipa hao, mkongwe Kaseja ni kama hatakiwi tena na timu hiyo,
kwani kitendo cha kumsajili kipa namba moja wa Kagera, Ntala huku Dhaira
akiwepo kikosini inaonyesha wazi mmoja kati ya Kaseja au Dhaira anatakiwa
kuondoka.
Dhaira
hadi anatua Simba alikuwa kipa wa kutegemewa wa timu ya taifa ya Uganda, The
Cranes, hata huyu Ntala naye ni tegemeo la Kagera. Hii ina maana wote hao sasa
wanatakiwa kupambana na Kaseja kuwania nafasi ya kwanza kikosini.
Ni
ngumu kwa Simba kuachana na Dhaira kwani mkataba wake ni mkubwa na ambao
unaweza kuigharimu Simba kiasi kikubwa cha fedha kuuvunja.
Popote
pale duniani, huwezi kusajili makipa namba moja wawili kutoka timu nyingine huku
tayari ukiwa na kipa hodari. Hii ni sawa na usajili mwingine wa nafasi nyingine
uwanjani.
Tayari
kuna tetesi kwamba, Simba ipo tayari kumwachia Kaseja ajiunge na klabu nyingine
kwa madai ya kushuka kiwango na kushindwa kuisaidia timu kushika moja kati ya
nafasi mbili za juu.
Mchakato
mzima wa kuhakikisha Kaseja anaondoka Simba unaongozwa na kiongozi mmoja ambaye
sasa ana sauti ndani ya klabu hiyo na mbaya zaidi hakuna sababu za msingi za
kumuacha Kaseja.
KUSHINDWA
KUISAIDIA SIMBA
Sababu
kwamba Kaseja ameshindwa kuisaidia Simba haingii akilini kutokana na ukweli
kwamba hata katika mechi ambazo Simba imefungwa Kaseja akiwa langoni, kuna vitu
vingi vilikuwa vinatokea.
Hadi
sasa hakuna hoja ya msingi iliyotolewa na uongozi juu ya mpango huo
unaotengenezwa wa kuhakikisha Kaseja anaondoka Simba kwa njia yoyote ile, bali
inayolazimishwa ni hii ya kushindwa kuisaidia timu.
Hawafafanui
jinsi kipa huyu alivyoshindwa kuisaidia Simba kushika moja kati ya nafasi mbili
za juu, kwani hajawahi kufungwa mabao manne katika mechi moja na idadi kubwa ya
kufungwa kwake katika mchezo mmoja haizidi mabao matatu.
HAKUWA
NA WASAIDIZI WA MAANA
Ikumbukwe
ya kwamba, Kaseja ni kipa imara anapokuwa na mabeki imara, sasa tazama ndani ya
msimu huu alikuwa na mabeki wa kati wa aina ipi na walikuwa na uwezo upi.
Msimu
wa 2011/12 ambao Simba ilitwaa ubingwa, kwa kiasi kikubwa Kaseja alilindwa na
mabeki Juma Nyosso na Kelvin Yondani, hao aliweza kuwapanga ipasavyo na ni safu
iliyokuwa ikielewana kwa muda mrefu.
Msimu
uliopita Kaseja amecheza na safu nyingi za ulinzi wa kati Victor Costa, Nyosso,
Shomari Kapombe, Komalbil Keita, Pascal Ochieng, Mussa Mudde hadi chipukizi
Hassan Khatib. Tazama mlolongo huo wa mabeki.
Utitiri
huo wa mabeki haukuweza kumsaidia Kaseja kwani ulikuwa ukibadilika kila mara na
mwisho wake hata kocha Patrick Liewig akawa anafanya kazi ya kujaribu mabeki
hadi ligi inaisha.
Tazama
kiungo Mudde aliyesajiliwa katika timu kama kiungo lakini kutokana na uhaba wa
mabeki, Simba ikaamua kumchezesha kama beki. Mbaya zaidi akachezeshwa katika
nafasi hiyo kwenye mechi muhimu kama ya Simba na Yanga.
KASEJA
ANAFUNDISHWA NA NANI?
Unaweza
ukaona kama utani lakini ndiyo soka lilivyo, kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ wa
Yanga aliichezea Simba msimu wa 2011/12, hakuwa akipata nafasi na hata
alipopewa nafasi alikuwa hafanyi vizuri kama ilivyo kwa Kaseja, ili lipo wazi.
Lakini
msimu uliopita, Barthez aliipa Yanga ubingwa na kutangazwa kuwa kipa bora wa
ligi nzima. Sababu zipo wazi.
Akiwa
Simba, Barthez alikuwa anapata mafunzo ya ugolikipa akiwa sambamba na Kaseja,
lakini alipotua Yanga ndani ya muda mfupi timu hiyo ikampa kazi Razack Siwa,
ambaye pia ni kocha wa makipa wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars.
Siwa
ni kipa wa zamani pia aliwahi kuinoa Yanga tena kwa nafasi zote mbili, kocha
mkuu na kocha wa makipa, kwa kifupi huyu amesheheni katika kufundisha makipa na
ameshasoma kozi kibao za kufundisha makipa.
Katika
mahojiano na kituo cha runinga cha Clouds kupitia kipindi cha Sports Bar, Siwa
aliwahi kusema tatizo la wakufunzi wengi wa makipa, wanafanya mambo ambayo
hayatokei uwanjani na wanashindwa kumuandaa kipa kuwa jasiri uwanjani.
Anatolea
mfano kwa mazoezi ya kuwarushia mipira makipa ili wadake, Siwa anasema hilo ni
tatizo kwani kipa akiwa uwanjani anapigiwa mashuti na wala harushiwi mipira na
wachezaji wa timu pinzani. Siwa huwapigia mashuti makali makipa wake katika
mazoezi.
Huo
ni mfano mdogo tu wa Siwa, lakini kuna vitu vingi ambavyo vinamfanya Barthez
aonekane anafanya vizuri uwanjani, lakini bado huyu ni yuleyule na Kaseja ni
yule yule.
Barthez
msimu wote huu amecheza chini ya mabeki Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’
na wakati mwingine Athuman Idd Chuji au Mbuyu Twite. Hao wote ni wachezaji
wazoefu. Hata hivyo muda mwingi walicheza Cannavaro na Yondani.
POULSEN
ANAWAKOSOA
Pamoja
na Simba kumuona wa nini, bado Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen anamuona
Kaseja ni kipa bora na ndiyo maana anaendelea kumuita kikosini na kumtumia pia.
Poulsen
siyo kwamba haoni vipaji vya makipa Mwadini Ally wa Azam FC na Barthez, kuna
kitu cha ziada anachohitaji kutoka kwa Kaseja ndiyo maana anamtumia kikosini.
Kitu
ambacho Poulsen amekiona kwa Kaseja ni uzoefu ambao haupo kwa Barthez au
Mwadini japokuwa wote wana viwango vinavyolingana.
SIMBA
HAITAKI KUWA NA GIGGS WAO?
Ukongwe
ndani ya timu ya soka ni moja kati ya vitu muhimu ambavyo klabu nyingi za Ulaya
na Afrika vinahitaji ili kuzifanya ziwe na maendeleo.
Kaseja
ameichezea Simba kwa zaidi ya miaka 10 sasa, maana tangu ajiunge nayo mwaka
2002 akitokea Moro United ameachana nayo mwaka mmoja tu alipotimkia Yanga.
Manchester
United inapohakikisha inabaki na mtu kama Ryan Giggs kikosini huwa inahitaji maendeleo
kwani damu changa peke yake si rahisi kuipa mafanikio. Wakongwe ndiyo
wanaotumiwa kuweka mambo sawa kati ya uongozi na klabu.
Yawezekana
Simba sasa inamuona Kaseja kama kikwazo cha wao kuwamiliki na kuwatumikisha itakavyo
wachezaji chipukizi tena kwa malipo hafifu, maana yawezekana wanamuona Kaseja
atawafuta mchanga machoni.
HAWAONI
YALIYOTOKEA KWA CASILLAS & MOURINHO
Ni
ukweli usiofichika kwamba, kipa Iker Casillas ndiye kila kitu kati ya wachezaji
wa Real Madrid na hata timu ya taifa ya Hispania. Kocha Jose Mourinho muda
mfupi baada ya kutua kuifundisha klabu hiyo alitaka kufuta hali hiyo kwa
Casillas.
Mourinho
alitaka yeye kuwa mtu muhimu katika timu kuliko Casillas, akamtengezea
mazingira kipa huyo ya kuonekana hafai na kuanza kumuweka benchi bila sababu ya
msingi.
Hata
hivyo, Madrid ni miongoni mwa klabu zinazothamini mchango wa wakongwe kama
Casillas ambao wanaweza kuisaidia timu ndani na nje ya uwanja. Ikaamua kuachana
na Mourinho ili ibaki na Casillas.
Ndiyo
maana Chelsea leo hii ina John Terry, Liverpool yupo Steven Gerrard, Man United
wanaye Giggs, na hata Yanga wanaye Shadrack Nsajigwa. Sasa iweje Simba imtimue
Kaseja?
Umefika
wakati sasa siasa na chuki zisizo na maana ziondoke katika mazingira ya soka
letu ili tuweze kufikia mafanikio.
0 comments:
Post a Comment