ZILE
NYAKATI za vikumbo vya Uhamisho wa Wachezaji kabla Msimu mpya kuanza
ndio zimepamba moto na Manchester City tayari wameshamnasa Staa wa
Brazil Fernandinho huku Staa mwingine wa Nchi hiyo, Hulk, akithibitisha
Chelsea kumuwania wakati huko Etihad zipo habari za Arsenal kumtaka
Kiungo wa Everton Marouane Fellaini.
HULK
Hulk, alipohojiwa, alijibu: “Nikisema
kuwa hamna lolote, nitakuwa nadanganya! Lakini haya si kwa sasa. Kwa
sasa nipo Aslimia 100 na Brazil na nategemea kushinda Kombe la Mabara!
Mengine yatasubiri hadi baadae!”
FELLAINI
Huko London, upo uvumi mzito kuwa Kiungo
wa Everton, Marouane Fellaini, huenda akachukuliwa na Arsenal ambao
inadaiwa wako tayari kulipa Pauni Milioni 24 ambalo ndio Dau lililopo
kwenye Mkataba wa Mbelgiji huyo ikiwa anataka kuvunja Mkataba na
Everton.
Ingawa imedaiwa sana kuwa Fellaini
atamfuata aliekuwa Meneja wake huko Everton, David Moyes, ambae sasa
yupo Manchester United, lakini uvumi huo wa Kiungo huyo kwenda Arsenal
unadai kuwa Old Trafford inasita kumchukua hasa kwa sababu ya staili
yake ya uchezaji iko tofauti na ile ya Klabu hiyo ingawa pia hilo hilo
linaweza kusemwa kwa staili ya Arsenal.
CITY YAMSAINI FERNANDINHO
Manchester City imekamilisha kumsaini Kiungo wa Klabu ya Ukraine Shakhtar Donetsk, Fernandinho, kwa kitita cha Pauni Milioni 30.
Fernandinho, mwenye Miaka 28 na ambae ameichezea Brazil mara 5, amesaini Mkataba wa Miaka minne.
Fernandinho anakuwa Mchezaji wa kwanza
kusainiwa na Man City katika Kipindi hiki ingawa pia wana makubaliano ya
kumchukua Winga wa Sevilla ya Spain, Jesus Navas.
Hadi sasa, Man City haina Meneja baada
ya kutimuliwa Roberto Mancini mwishoni mwa Msimu ulioisha Mei lakini
inatarajiwa Wiki ijayo Meneja wa Klabu ya Spain Malaga, Manuel
Pellegrini, atatangazwa rasmi kuwa Meneja wao mpya.
FERNANDINHO:
-Jina kamili: Fernando Luis Roza
-Klabu: Atletico Paranaense (2002-2005); Shakhtar Donetsk (2005-2013)
-Mechi: 385
-Magoli: 68
-Brazil: Mechi 5
Akiongelea Uhamisho wake, ambae inadaiwa
alisamehe Pauni Milioni 4 za Mkataba wake na Shakhtar Donetsk ili
ahamie Man City, alisema: “Lengo langu hapa ni kutwaa Ubingwa! Hapa ipo
Timu imara, Klabu bora na Mashabiki ni wazuri! Kuchezea Klabu kubwa
katika Ligi kubwa kutanipa furaha! Nitalipa fadhila!”
0 comments:
Post a Comment