Tuesday, June 11, 2013

AKIWA DARAJANI JOSE MOURINHO ATAKA KUITWA MTU SPESHO

ATANGAZA KUTOSAINI LUNDO LA WACHEZAJI ILA MMOJA, WAWILI TU!
MOURINHO_KILIOYULE MENEJA alietua Chelsea mara ya kwanza na kujibatiza ‘MTU SPESHO’, Jose Mourinho, leo akitambulishwa rasmi kama Meneja mpya ametamba sasa aitwe ‘MWENYE FURAHA’ kwani ni Meneja mtulivu na bora kupita alivyokuwa.
Mourinho, mwenye Miaka 50 na aliwahi kuwepo Chelsea kati ya Mwaka 2004 na 2007, alitangazwa rasmi kuwa Meneja mpya wa Chelsea hapo Juni 3.
Leo akiongea na Wanahabari alisema: “Sasa ni ‘Mwenye Furaha!’ Mtulivu? Naamini ndio. Nipo katika wakati bora wa maisha yangu kwa vile nina uzoefu zaidi. Nilianza kuwa Meneja Mwaka 2000. Nilidhani najua kila kitu lakini baada ya Miaka 13 unagundua hujui lolote na inabidi ujifunze kila Siku. Uzoefu wangu wa Ulaya ni kitu safi, Nchi tofauti, Utamaduni tofauti, Vyombo vya Habaro tofauti. Ni kitu chema! ”
Aliongeza: “Nikiwa na Miaka 50 bado ni Kijana kama Meneja na nadhani ni mwanzo wa Kipindi kipya. Nimebadilika? Hapana , uhakika ni kuwa sasa nina mtazamo tofauti!”
Mourinho, ambae amembadili aliekuwa Meneja wa Muda Rafael Benitez, amesaini Mkataba wa Miaka minne na Chelsea.
Leo alidai: “Nategemea kufika hadi Siku ya mwisho ya Mkataba wangu. Ikiwa Klabu ina furaha na Klabu itataka nibaki basi mie nitabaki kwa furaha.”
Alipohojiwa kama alivunjika moyo kwa kutofuatwa na Manchester United au Manchester City kuwa Meneja wao, Mourinho alijibu: “Nipo hapa ambako nilitaka kuwepo-sitabadili chochote kwa hili!”
Akiwa na Chelsea kwa mara ya kwanza, Mourinho alifanikisha kutwaa Mataji matano ambayo ni Ubingwa wa Ligi, mara 2, Ligi Cup, mara 2 na FA CUP.
Jose Mourinho-Vikombe:
Champions League: 2004, 2010
Uefa Cup: 2003
Primeira Liga (Portugal): 2003, 2004
Premier League (England): 2005, 2006
Serie A (Italy): 2009, 2010
La Liga (Spain): 2012
Taca de Portugal: 2003
FA Cup (England): 2007
Coppa Italia (Italy): 2010
Copa del Rey (Spain): 2011
Mourinho pia alisema: “Nataka niamini kuwa inawezekana- Siku zote naamini Kazi yangu. Nawajua Watu wengi hapa na najua nini msimamo wao na wanachopigania. Maisha yangu kama Meneja yamejengwa na mafanikio. Nimeweza kupata mafanikio na kushinda Vikombe katika kila Klabu niliyokuwepo. Lazima niamini hilo!”
Akifafanua jinsi alivyotimka Chelsea Mwaka 2007 huku wengi wakijua ni baada ya kugombana na Mmiliki Roman Abramovich, Mourinho alieleza: “Hilo si kweli. Nilisoma na nimeendelea kusoma nilifukuzwa na nilivunja uhusiano kabisa. Wakati ule, pande zote mbili tuliona ni bora kutengana na kwenda njia zetu tofauti. Ulikuwa uamuzi mgumu lakini ni uamuzi uliofanywa kwa makubaliano ya wote. Na ndio maana leo nipo tena hapa!”
Vile vile Mourinho alitamka anataka kumfanya Beki wake John Terry "kuwa Mchezaji Bora tena.
Chelsea managers under Roman Abramovich
-Claudio Ranieri: Sep 2000 to Mei 2004
-Jose Mourinho: Juni 2004 to Sep 2007
-Avram Grant: Sep 2007 to Mei 2008
-Luiz Felipe Scolari: Jul 2008 to Feb 2009
-Guus Hiddink: Feb 2009 to Mei 2009
-Carlo Ancelotti: Jun 2009 to Mei 2011
-Andre Villas-Boas: Jun 2011 to Machi 2012
-Roberto Di Matteo: Machi 2012 to Nov 2012
-Rafael Benitez: Nov 2012 to Mei2013
-Jose Mourinho: Juni 2013 - sasa
John Terry, Miaka 32, Msimu uliopita alizokosa Mechi nyingi kwa kuwa Majeruhi na pia Kufungiwa lakini hata alipokuwa fiti na anaweza kucheza, Meneja Rafael Benitez alikuwa hampangi.
Na Mourinho ametamka: “Sitasema neno lolote kuhusu maamuzi ya Rafael Benitez, kuhusu Terry au Mchezaji mwingine yeyote. Natarajia kukutana na Terry Julai 1 na kujaribu kumfanya awe tena Mchezaji bora.”
Akizungumzia Kikosi chake, hasa Wachezaji ambao alikuwa nao alipokuwepo Stamford Bridge kwa mara ya kwanza, Mourinho alieleza: “Bado wapo Wachezaji wachache tangu wakati wangu ule, na ni muhimu kukueleza wewe, na si wao kwa sababu wanajua hilo, hamna upendeleo kwa wao. Wanajua tabia yangu. Sipendelei Mtu na wao hawatapendelewa zaidi ya wengine.”
Vile vile Mourinho aliwajulisha Mashabiki kuwa wasitegemee kuona Wachezaji wengi wapya wanasainiwa ingawa watakuwepo wachache wapya.
Alisema: “Inabidi tufanye kazi na Wachezaji waliokuwepo na baada ya hapo tutaamua. Kusaini Wachezaji wawili hivi ni kawaida, na ni kitu sawa kwa kila Klabu.”

0 comments:

Post a Comment