Wednesday, February 5, 2014

Wabunge majangili sasa imekula kwao!!!!!











Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu. PICHA|MAKTABA 
Serikali imetangaza rasmi kuanza upya kwa ‘Operesheni Tokomeza Majangili’, baada ya kuisitisha zaidi ya miezi mitatu iliyopita kutokana na operesheni hiyo kukumbwa  na matatizo ya utekelezaji  ambapo vilitokea vitendo vya ukatili na mateso .............
na kuwaacha raia 13 na askari 6 wakiwa wamepoteza maisha. Matukio hayo ya kusikitisha yalisababisha mawaziri wanne kupoteza nyadhifa zao serikalini baada ya Kamati ya Bunge ya Maliasili na Utalii iliyoundwa kuchunguza vitendo hivyo kuwasilisha taarifa yake bungeni.
Ni vyema tukakiri hapa kwamba awamu ya pili ya operesheni hiyo inaonyesha dalili za mafanikio hata kabla haijaanza, kwani Serikali inaonekana imejizatiti ipasavyo kwa kuweka utaratibu wa kuratibu na kutekeleza operesheni hiyo ili kasoro zilizojitokeza katika awamu ya kwanza zisirudiwe,   pia kwa kuonyesha bayana kuelewa ukubwa wa tatizo na changamoto itakazopambana nazo wakati wa utekelezaji. Hii ni pamoja na kubuni mbinu na mikakati mipya ya utekelezaji na kuhakikisha zoezi zima linaendeshwa kwa kuzingatia haki za binadamu.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema juzi wakati akitangaza kuanza kwa operesheni hiyo kuwa, Serikali inatambua kwamba inapambana na watu wenye nguvu kubwa, ikiwa ni pamoja na majangili na wafadhili wa mtandao wa biashara ya pembe za ndovu. Alisema watawakamata kuanzia maporini, ofisini na hata majumbani. Hiyo ni kauli nzito inayoashiria kwamba Serikali mara hii pengine inayo dhamira ya kweli ya kutokomeza vitendo vya ujangili katika hifadhi za Taifa, kwani operesheni iliyopita ilihujumiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na Serikali, ambao wao binafsi ama ndugu zao walikuwa wakihusishwa na ujangili.
Miezi mitatu sasa baada ya kusitisha operesheni ya awali, tuhuma bado zimepamba moto kwamba mikakati ya kuwang’oa mawaziri ambao wizara zao zilihusika katika utekelezaji wa operesheni hiyo zilisukwa na baadhi ya wabunge waliokuwa wakihusishwa na ujangili, huku wengine kadhaa wakidaiwa kufanya hivyo kwa masilahi binafsi ya kisiasa.
Kutokana na Kamati ya Kudumu ya Bunge kuliambia Bunge kwamba inayo majina ya wabunge na wanasiasa wanaotuhumiwa kujihusisha na ujangili, wananchi wengi sasa wanataka operesheni hiyo mpya isianze kabla majina ya watu hao hayajawekwa wazi, vinginevyo operesheni hiyo itaonekana kama kiini macho.
Ni kwa sababu hiyo tunaitaka Serikali mara hii isiwe na mzaha katika kuendesha operesheni ijayo. Kwa upande mmoja iwaondoe wakulima na wafugaji ndani ya hifadhi, kwani nchi yetu inayo ardhi ya kutosha nje ya hifadhi hizo kwa shughuli za kilimo na ufugaji. Ukweli ni kwamba wananchi hao ndiyo mawakala wa majangili wakubwa wanaomaliza tembo na maliasili nyingine. Pili ihakikishe  makazi ya watu yako mbali na hifadhi, kwani imegundulika wengi wa wafanyabiashara na wanasiasa wanaoishi karibu na hifadhi hizo nchi nzima wanajihusisha na ujangili na kwa kiasi kikubwa ndiyo waliofadhili njama za kuihujumu operesheni iliyopita.
Wakati tukisubiri uundwaji wa Tume ya Kimahakama kushughulikia ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa  operesheni ya awali, tunawataka wanasiasa, wakiwamo wabunge waiache Serikali itekeleze wajibu wake katika operesheni itakayoanza hivi punde. Baadhi ya wabunge waliopinga operesheni hiyo wanahusika na ujangili. Pengine ndiyo maana wananchi hawana tena shauku ya kuona Tume  ya Kimahakama ikiundwaPosted http://thesuperonenews.blogspot.com/.

0 comments:

Post a Comment