Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amesema mchakato wa kuwapata wajumbe wa Tume ya Kimahakama ya Kuchunguza Madhara ya Operesheni Tokomeza Ujangili umeshaanza na majina hayo yatawekwa wazi hivi karibuni.
Jaji Werema alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo unahitaji umakini mkubwa na majina hayo lazima yakubaliwe na Rais, kabla ya kutangazwa.
Baadhi ya vifungu vya sheria hiyo vinasema kuwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ana uwezo wa kuteua ofisa wa polisi kuwemo kwenye tume hiyo, kushauriana na Rais kuhusu wajumbe hao na wajumbe wa tume hiyo kwa sababu wanatoka katika Jeshi la Polisi wanaweza.
Kadhalika sheria hiyo inaelekeza kila mjumbe wa tume kula kiapo mbele ya Rais kabla ya kuanza kazi.
Ripoti ya Bunge
Baada ya ripoti hiyo kusomwa bungeni Desemba mwaka jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, Rais Jakaya Kikwete aliamuru iundwe tume ya kimahakama ili kuchunguza ukweli wa ripoti hiyo pamoja na waliotajwa kuhujumu operesheni hiyo.
Kabla ya kuhamishwa wizara, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alisema mchakato wa kuundwa kwa tume hiyo ya kimahakama huenda ukakamilika mwezi huu.
Chikawe alisema, Tume hiyo itaundwa na jaji kutoka Mahakama Kuu, wapelelezi na baadhi ya wanasheria.
“Itahusisha watu ambao watafanya kazi kisheria zaidi kwa kuangalia kwa kina kipi kilitokea wakati wa operesheni hiyo, ili tuufahamu ukweli kwa sababu ripoti ile kwa kweli ilitushitua,” alisema Chikawe.
Alisema tume hiyo itapita katika maeneo yote ambayo yametajwa kwenye ripoti na kufanya uchunguzi wa kina kubaini iwapo kweli matukio kama hayo yalifanywa na polisi.
“Pia tume itajaribu kuangalia kama ni kweli wapo watu ambao walikuwa wanapata yale mateso yaliyotajwa kwenye ripoti kwa mfano mtu kulazimishwa kuchora chatu kwa kutumia kiwembe kwenye paja,” alisema.
Chikawe alisema kama tume hiyo itagundua kuwa ni kweli polisi walifanya unyama huo basi kwa hakika hatua kali zitachukuliwa. Posted by http://thesuperonenews.blogspot.com/
0 comments:
Post a Comment