Friday, January 24, 2014

SAKATA LA OKWI : FIFA YATOA SIKU TANO TU!!!!


SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa) limeipa Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia hadi Januari 27, kuanzia jana liwe limetoa maelezo ya uhakika kuhusiana na usajili wa Emmanuel Okwi. la sivyo watamsahau!!!!! 

Usajili wa Okwi umezua utata mkubwa na kuzigonganisha timu nne kutoka katika nchi za Afrika Mashariki na Afrika Kaskazini.

Simba, Yanga za Tanzania, SC Villa ya Uganda (zote kutoka Afrika Mashariki) na Etoile ya Afrika Kaskazini, kila upande uko ndani ya mgogoro wa mchezaji huyo mmoja.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amesema Fifa imetoa agizo hilo huku ikisisitiza inataka kujua kuhusiana na malipo ya Mganda huyo kutoka Simba kwenda Etoile.
Ikiwa ndiyo siku moja tu tangu Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF kusitisha usajili wa Okwi Yanga, Rage amesema amepokea ujumbe kutoka Fifa ambao unaitaka klabu hiyo ya Tunisia kutoa maelezo hayo.
Simba inadai dola 300,000 (Sh milioni 480) ilizomuuza Okwi kwa Etoile na hadi leo imekuwa ‘ikiingia huku na kutokea kule.’
“Tumefarijika sana na taarifa hiyo, tunajua haki lazima itatendeka, maana awali baadhi ya watu wa Simba waliamini kuwa nilikula fedha ya Okwi,” alisema Rage.
Rage ndiye alihusika katika mauzo ya Okwi na amekuwa akilaumiwa kwa kushindwa kufanya mchahato huo kwa njia ambayo ingeipatia Simba fedha kwa wakati mwafaka.
Aliongeza kuwa, Simba haina shida na Okwi ila wanachohitaji ni malipo yao na kudai kuwa walikubaliana atakapokuwa anauzwa, Simba itapata mgawo wa asilimia 20 za usajili, hivyo anashangaa mpaka sasa anaichezea Yanga, wakati wao Simba hawajapata mgawo wowote.
Gazeti hili lilipomuuliza Katibu wa Yanga, Beno Njovu juu ya sakata la Okwi kuzuiwa kuichezea timu yao, alisema: “Sisi pia tunasikia kupitia vyombo vya habari, kama ni mchakato tulifanya kihalali, tuna uhakika na tulichokifanya, tunasubiri barua rasmi kutoka TFF kisha tutatoa tamko.”
Aidha, Rage ametangaza mabadiliko katika sekretarieti ya Simba, ambapo Ezekiel Kamwaga ameteuliwa kuwa katibu mkuu, akisaidiwa na Stanley Phillip kama Katibu Msaidizi huku Asha Muhaji akiteuliwa kuwa Ofisa Habari.
Wengine ni Eric Kiete (Mhasibu), Hussein Mzei (Ofisa Utawala), Amina Kumwambe (Ofisa Utawala Msaidizi) na Issa Juma Matayo   (mwangalizi wa ofisi) 

0 comments:

Post a Comment