Sunday, July 28, 2013

HAUSIBOI ALIYEMLAWIT BINTI WA MIAKA MINNE YAMKUTA MAKUBWA MAHAKAMANI


Mahakama  ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi imemhukumu kijana, Baraka  Juma (22) mkazi wa kijiji cha Nkungwi  wilayani humo, kifungo cha maisha jela  baada ya kupatikana  na hatia  ya  kosa la kumlawiti mtoto wa kike mwenye umri  wa  miaka minne  baada  ya kumhadaa na  kumlewesha bia.

Akisoma  hukumu  hiyo  juzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Chiganga Tengwa  alisema ameridhishwa  na  ushahidi  pasipo kutia shaka uliotolewa mahakamani hapo na upande zote  mbili za mashitaka na utetezi.
 

“Nimelazimika kutoa adhabu  kali  kwa mshtakiwa  baada ya  mahakama  hii kumtia  hatiani  ili  iwe  fundisho  si kwake  tu, lakini  pia  kwa wengine  wenye tabia  kama  yako .... kitendo  ulichomtendea mtoto  huyo  ni  cha kinyama hustahili  kuonewa  huruma, “ alisema Tengwa.

Awali Mwendesha Mashitaka, Mkaguzi wa Polisi, Lazaro Masembo alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Aprili 2 mwaka huu nyumbani kwa wazazi  wa mtoto huyo ambako mtuhumiwa  alikuwa ameajiriwa na wazazi wake kama mfanyakazi wa ndani.

Ilidawa  mahakamani  hapo  kuwa siku hiyo  ya tukio mama mzazi wa mtoto huyo alikuwa amekwenda kijiji cha jirani kutembelea ndugu zake  ambapo  alimwacha mtoto  wake huyo  chini  ya  uangalizi wa mshitakiwa.
 


Pia  nyumbani hapo  ilidaiwa  mahakamani  hapo  kuwa  kulikuwa  na  msichana  aitwaye Nyasolo Doya (18 ) ambaye  alikuwa  mgeni wa  nyumba hiyo ambaye alifikia hapo  kujifungua.

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka, Masembo,  mtuhumiwa alimwita mtoto huyo  sebuleni ambako  alikuwa  amekaa na kisha akaanza  kunywesha  bia aina ya  Balimi  kisha  akamlawiti  huku  mtoto akipiga kelele kwa maumivu akisikika akisema, “mama  nakufa.”

Mahakama  hiyo  ilielezwa  kuwa  kufuatia  kelele za  kilio  cha mtoto  huyo, msichana  Nyasolo Doyo  alishtuka na kulazimika  kukimbilia  sebuleni  ndipo alipomshuhudia  mshitakiwa akimwingilia mtoto  huyo huku akiwa amevua  nguo zake.


Mwendesha Mashtaka Masembo  alisema Nyasolo alipomsihi Baraka amwachie  mtoto  huyo aligeuka ‘mbogo' na kumtishia  kuwa iwapo atatoa  siri  hiyo kwa wazazi wa mtoto  huyo  atamuua, ndipo  msichana huyo aliponywea kwa hofu  ya tishio  hilo  la  kuuawa.

Mahakama hiyo  ilizidi kufahamishwa kuwa  mama mzazi wa mtoto huyo alirejea nyumbani kwake saa mbili usiku  na ndipo  alipomwona binti yake  huyo akitembea kwa kuchechemea  mwendo  uliomshtua  mama  huyo  na akaamua  kumuuliza msichana Nyasolo  ambaye  alimsimulia mkasa wote  huo wa kusikitisha.

 

Mwendesha Mashtaka alidai  mahakamani hapo kuwa  mama huyo  alilazimika kumpigia simu baba mdogo wa mtoto huyo ambae anaishi kijiji cha jirani ambae alifika  nyumbani  hapo saa nane usiku na ndipo walipoamua kumfungia mtuhumiwa  mlango wa chumba chake kwa nje na kisha walienda kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji.
 


Katika shauri hilo upande wa  mashtaka ulikuwa na mashahidi  watano mmojawapo akiwa daktari aliyemfanyia  uchunguzi wa kitabibu mtoto huyo na kuthibitisha  kuwa   alikuwa ameingiliwa na mwanaume katika sehemu zake za siri ambapo  mshitakiwa hakuwa na shahidi yeyote.
 

Katika utetezi wake, mshitakiwa aliiomba mahakama imwachie huru kwa kile alichokieleza kuwa alisingiziwa tu.

0 comments:

Post a Comment