Monday, October 28, 2013

PELLEGRINI ASUSA KUPEANA MKONO NA MOURINHO!

PELLEGRINI-KIDOLE

MENEJA wa Manchester City Manuel Pellegrini, Jana mara baada ya Timu yake kuchapwa Bao 2-1 huko Stamford Bridge na Chelsea kwenye Mechi ya Ligi Kuu England, alitokomea kwenye Vyumba vya Kubadilishia Jezi bila ya kupeana mkono na Meneja wa Chelsea Jose Mourinho.
>>NI BAADA KICHAPO CHA CITY 2-1 TOKA CHELSEA, STAMFORD BRIDGE!
Chelsea walishinda Mechi hiyo kwa Bao la Dakika ya 90 la Fernando Torres ambalo lilimfanya Mourinho ashangilie kichizi na kupanda Jukwaa la Watazamaji na kujumuika nao kushangilia.
Baada ya Mechi, kwenye Mahojiano na Wanahabari, Pellegrini alisema: “Sikupeana mikono. Sikutaka kufanya hivyo.”
Hata hivyo, Mourinho aliomba radhi kwa ushangiliaji wake na kudai alikuwa akijaribu kumtafuta Mtoto wake wa Kiume.
Amesema: “Kama wanahisi nimefanya kosa, naomba radhi. Hii ni shamrashamra ya Bao la Dakika ya mwisho. Yeye [Pellegrini] amepoteza Mechi Dakika ya mwisho na namwonea huruma kwa hilo. Katika Nchi nyingine tunapeana mikono kabla ya Mechi, na basi. Kama alihuzunishwa na kufungwa, ninamwelewa. Na kama amehuzunishwa kwa kosa langu basi nakubali kosa.”
Mourinho na Pellegrini wana bifu lao tangu huko Spain ambako Mwaka 2010 Mourinho ndio alimbadili Pellegrini kama Kocha wa Real Madrid baada ya kuondolewa kwa kushindwa kuipa Ubingwa Real na kumaliza Nafasi ya Pili nyuma ya Barcelona na Kocha huyo akajiunga na Malaga.
Wakati huo, Mourinho alibatuka: “Nafasi ya Pili ni Timu ya Kwanza kufungwa. Kama Real wangenifukuza mimi, nisingekwenda Malaga! Ningekwenda kwenye Timu kubwa huko Italy au England!”

0 comments:

Post a Comment