KOCHA Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio,’ amesema Haruna Moshi ‘Boban’ bado ni mchezaji mzuri kama akiamua kucheza soka, na kuwa hajashuka uwezo wake.
Kihwelo, beki wa zamani wa Simba na Taifa STARSalisema kuwa kiungo huyo aliyemaliza mkataba wake na Simba, akiamua kucheza soka atakuwa na msaada mzuri kwa timu yake ya Coastal Union na Taifa Stars kwani bado ana uwezo mkubwa wa kucheza soka.
“Boban bado ni mchezaji mzuri, akiamua kucheza soka hakuna mchezaji yeyote wa kumlinganisha naye kwa Tanzania katika nafasi yake, akiamua atakuwa na msaada kwa Coastal Union na Taifa Stars,” alisema Julio kumzungumzia kiungo huyo anayehamia Coastal Union msimu ujao akitokea Simba.
Alisema Simba haijamuongeza mkataba kwa sababu ya uwezo wake, bali kwa kuona kuwa kiungo huyo hataki tena kucheza soka na kusema kwa kuwa amejiunga na Coastal Union, inaonesha ameamua kucheza.
“Kwa kuwa ameamua kusajili Coastal Union inaonesha kuwa ameamua na anataka kucheza soka atawasaidia na atalisaidia Taifa, Simba haijamuongeza mkataba kwa sababu ilimuona hataki kucheza soka, lakini sio kuwa hana uwezo,” alisema Kihwelo.
Julio alisema mara zote kiungo huyo mwenye kipaji cha hali ya juu akiamua kucheza soka anafanya hivyo na kumshangaza kila mtu kwa uwezo wake uwanjani.
“Unakumbuka kuna kipindi alikuwa anapigiwa kelele aitwe kwenye kikosi cha Taifa Stars na kocha Marcio Maximo alipomuita, alionesha uwezo mkubwa na kutengeneza bao alilofunga Abdi Kassim dhidi ya Uganda,” alikumbusha Julio.
Simba imeachana na nyota wake wengi wazoefu wakiwemo Boban, Amir Maftah, Ramadhani Chombo, Juma Nyosso na Komanbil Keita kwa sababu za utovu wa nidhamu na tayari kiungo Boban ameshasaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea Coastal Union ya Tanga katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Kutokana na kuachana na wakongwe hao, Simba imesajili nyota wengi chipukizi kutoka kikosi cha pili cha timu yake na timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu.
Baadhi ya nyota hao ni Edward Christopher, Ramadhani Singano, Haruna Chanongo, Jonasi Mkude, Ismail Mkoko, Wiliam Lucian. Wengine ni Armandus Nesta, Andrew Ntalla kutoka Kagera Sugar na wengineo.
0 comments:
Post a Comment