Friday, June 7, 2013

Udhaifu wa Wabunge bungeni waonekana.

makinda
SPIKA wa Bunge bi Anna Makinda amesema wabunge wengi wamepungukiwa uwezo kutokana na kuacha kuzungumzia mambo muhimu badala yake wanajadili watu binafsi. Aidha Mbunge wa kuteuliwa James Mbatia (NCCR Mageuzi ) amesema wabunge wengi ni wafungwa watarajiwa na ameomba magereza yaboreshwe maana wengi wataenda huko kutokana na kushiriki kushabikia na kupitisha mambo ambayo hayana maslahi kwa taifa.
Akizungumza juzi muda mfupi kabla ya kuahirisha shughuli za bunge baada ya kupitisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2013/2014 ya ,Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Spika Makinda alisema yapo mambo yanafanywa na baadhi ya wabunge ambayo wananchi hawapendi kuyasikia na hayafai.
“Wabunge tumepungukiwa badala ya kujadili ishu, sisi tunajadili watu binafsi,” alisema na kuongeza kuwa suala la wabunge kushambuliana wenyewe si kitu ambacho wananchi wanataka kukisikia na kusisitiza kuwa walio wengi wamepungukiwa.
Pia alimuomba Waziri wa Elimu na Mafunzo ya ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kuchukua changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwa wizara yake katika michango ya wabunge na kuifanyia kazi. Mbatia “Wabunge wengi ni wafungwa watarajiwa, naomba magereza yaboreshwe maana wengi wataenda huko kutokana na kushiriki kushabikia na kupitisha maambo ambayo hayana maslahi kwa Taifa.
“Ni suala linalosikitisha kuona wabunge wanakuwa chanzo cha mambo yasiyo na faida, hivyo nawaambia wajiandae, historia itatuhukumu, ni vyema tukabadilika na kuweka mbele maslahi ya Taifa badala ya ubinafsi,” alisema Mbatia.
Bajeti kupitiwa Wizara zote zimekamilisha kazi ya kusoma bajeti zake bungeni na leo Kamati mpya ya Bunge inayoshughulika mambo ya Bajeti inaanza kazi yake itakapokutana na mawaziri kwa ajili ya kupitia bajeti ya Serikali.
Kazi za kamati hiyo mpya inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge itafanya majumuisho kuzingatia hoja zenye maslahi kwa taifa zilizojitokeza wakati wa kujadili mapato na matumizi ya wizara mbalimbali.
Miongoni mwa wizara ambazo mapato na matumizi yake yalipingwa ni Wizara ya Maji ambayo wabunge waliungana kuikataa hali iliyofanya serikali kwenda kufanya marekebisho. Wizara hiyo ililalamikiwa na wabunge wengi kwa vile maeneo mengi ya nchi hayana maji hali inayozua malalamiko kwa wananchi.
Kwa hali hiyo wabunge waligoma kuunga mkono hoja ya waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe hali ambayo ilimlazimu kwenda kufanya mabadiliko. Wizara nyingine ambayo wabunge walichachamaa zaidi ni Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ambayo inaelezwa inatengewa fedha kidogo wakati majukumu yake yanamgusa zaidi mwananchi.
Kutokana na udogo wa bajeti ya wizara hiyo, mambo mengi yameshindwa kufanyika, wakati sera ya CCM inaelekezakuwa lengo la Serikali ni kuhuisha ufugaji ili waweze kuwa wafugaji wa kisasa kuliko ilivyo sasa.
Kwa upande wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo bajeti yake ilipitishwa juzi, pia baadhi ya wabunge wamelalamika hatua ya nusu ya bajeti yote kwenda Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu huku kiasi kilichobaki, kikitajwa kwamba ni kidogo kisichokidhi mahitaji.
Bunge ambalo lilianza kikao chake Aprili 8 mwaka huu pamoja na kamati hiyo kuanza kazi yake, leo kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe watakaowakilisha Bunge katika Taasisi/Vyuo mbalimbali.
Hotuba ya bajeti ya Serikali itasomwa na Waziri wa Fedha William Mgimba Alhamisi ijayo na itajadiliwa kwa siku tano.

0 comments:

Post a Comment