ASEMA HAKUTANGAZA MAPEMA KWANI KILA MTU ALIKUWA AKISTAAFU!!
MCHEZAJI
wa zamani wa Manchester United, Everton na Timu ya Taifa ya England
Phil Neville ametangaza kustaafu kucheza Soka baada ya Miaka 18 ya kuwa
Mchezaji.
Neville ametoboa kuwa atakuwa Mchambuzi
wa BBC, Shirika la Habari la Uingereza, kwenye Fainali za Kombe la Dunia
Mwaka 2014 huko Brazil.
Phil Neville-Mataji:
[Yote akiwa na Manchester United]
FA Youth Cup: 1995
Premier League: 1996, 1997, 1999, 2000, 2001, 2003
FA Cup: 1996, 1999, 2004
Community Shield: 1996, 1997, 2003
Champions League: 1999
Intercontinental Cup: 1999
Neville,
aliechezea England mara 59, alianza kucheza BPL, Barclays Premier
League, Mwaka 1995 akiwa na Manchester United katika Mechi dhidi ya
Manchester City na kushinda Bao 3-0 na akadumu Misimu 19 kwenye BPL.
Akiwa na Man United alitwaa Ubingwa wa
BPL mara 6, FA CUP mara 3 na Ubingwa wa Ulaya mara moja kabla kujiunga
na Everton Mwaka 2005.
Akiwa Everton, Phil Neville, chini ya Meneja David Moyes ambae sasa amehamia Man United, aliteuliwa kuwa Nahodha wa Klabu hiyo.
Neville pia alisema kuwa alishindwa
kutangaza kustaafu kwake Soka mapema kwa vile wakati huo huo Watu
aliokuwa nao kwa muda mrefu, Meneja wa Man United, Sir Alex Ferguson,
Wachezaji wenzake alioanza nao, David Beckham na Paul Scholes, wote
walitangaza kustaafu na yeye hakutaka kuonekana kufuata mkumbo.
Alisema: “Wiki 3 zilizopita, kila Mtu Duniani alionekana kustaafu! Mimi sikutaka nionekane nafuata mkumbo!”
Hivi sasa Phil Neville yupo mbioni
kumalizia kutwaa Leseni ya UEFA ya Ukocha kiwango A na alithibitisha ni
Sir Alex Ferguson ndio aliwataka wachukue Kozi za Ukocha na walipokuwa
Man United yeye na Roy Keane, Gary Neville, Nicky Butt na Ryan Giggs,
wote walichukua Mafunzo ya kiwango cha UEFA cha Leseni B ya Ukocha.
Neville aliongeza: “Tukiwa Man United,
Sir Alex Ferguson alitupa fundisho kubwa na kusisitiza tuanze Mafunzo ya
Ukocha mapema huku akituambia hamna njia ya mkato ya kuwa Meneja au
Kocha!””
Hivi sasa zipo habari kuwa Phil Neville
atakuwa mmoja wa Wasaidizi wa Meneja mpya wa Man United, David Moyes,
kama mmoja wa Makocha kwenye Benchi lake la Ufundi.
Akiwa Man United, Phil Neville alicheza
pamoja na Kaka yake Gary Neville ambae nae ameshastaafu na sasa anafanya
kazi kama Mchambuzi wa Soka kwenye TV ya SkySports.
Akiwa Beki wa Manchester United, Gary
Neville, Miaka 35, aliamua kutundika daluga zake Mwaka 2011 baada ya
kuichezea Man United tangu Mwaka 1992 na kucheza mechi 602 na pia
kuichezea Timu ya Taifa ya England mara 85.
Akitangaza kustaafu, Gary Neville
alitamka: “Mimi ni shabiki wa Man United maisha yangu yote na nimetimiza
kila ndoto yangu. Inaumiza ukitambua siku zako za kucheza zimefika
mwisho. Lakini mwisho hutufikia sote na ni bora kujua wakati umefika na
kwangu wakati huo ni sasa!”
Gary Neville alisaini kuichezea Man
United Julai 1991 na kucheza mechi yake ya kwanza Septemba 1992 kwenye
Kombe la UEFA Man United walipocheza na Torpedo Moscow.
0 comments:
Post a Comment