Saturday, June 8, 2013

KIJANA ALIYEDAIWA KUFANYA UTAPELI KANISANI NA MSIKITINI NCHINI AWEKWA CHINI YA ULINZI



KIJANA mmoja anayedaiwa kutapeli misikitini na makanisani sehemu mbalimbali nchini, William Daudi (pichani),  mkazi  wa Majengo mkoani Katavi amenaswa mjini hapa Jumanne iliyopita.
 Kijana William ambaye anadaiwa kufanya kazi ya  utapeli katika majengo ya ibada anapokuwamisikitinihutumia jina la Hassan Idd Lumbanga ambalo ni la bandia.
Siku zote za mwizi ni arobaini basi zilitimia kwa kijana  huyo baada ya siku hiyo kufika katika Msikiti wa Ijumaa Miyomboni akaungana na  waumini katika swala iliyokuwa ikiongozwa na Naibu Imamu  wa Msikiti, Issa Boki, ghafla  (kijana  huyo) alijiangusha  chini na kujifanya amepoteza fahamu .
Naibu Imamu Boki aliliambia gazeti hili kuwa iliwalazimu  kusitisha shughuli za ibada na kutafuta gari harakaharaka na wakamkimbiza kijana huyo katika hospitali ya mkoa ili akapatiwe tiba.
“Tulimuacha hapo hospitali kwani alilazwa lakini baada ya sisi kuondoka alianza kufanya fujo akahamishiwa wodi ya wenye mtindio wa ubongo, ambako nako alifanya vurugu,” alisema Boki.
Akifafanua zaidi, kiongozi huyo alisema walishitukia kijana huyo akiwa amerudi msikitini na kuanza kuomba msaada wa nauli akidai anataka kurudi kwao Katavi.
“Alichangiwa shilingi hamsini na tano elfu na mia mbili (55,200) wakati tunajiandaa kumpatia mmoja wa waumini wetu alimtambua kuwa alimuona jijini Dar es Salaam katika msikiti mmoja na akafanya kama alivyotufanyia sisi,” alisema Boki.
Naye Katibu  wa Msitiki,  Juma Kibasila alisema baada ya madai hayo, walimhoji kijana huyo na akakiri kuwa yeye ni tapeli na kwamba amekuwa akiishi kwa njia hiyo na walipompekua walimkuta akiwa na funguo nyingi, hivyo kumkabidhi kwa polisi wa kituo cha kati ambako aliwekwa korokoroni akisubiri upelelezi.

0 comments:

Post a Comment